UFATILIAJI WA AGENDA 2030 UNAHITAJI TAKWIMU SHIHI-TANZANIA
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema takwimu
sahihi zitahitajika katika kufuatilia utekelezaji wa Malengo ya
Maendeleo Endelevu maarufu kama Agenda 2030.
Hayo yameelezwa siku ya jumatano na Mwakilishi wa Kudumu
wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati
wa Mkutano wa 49 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Idadi ya
Watu na Maendeleo ( CPD), mkutano unaoendelea hapa
Umoja wa Mataifa.
Balozi Manongi anayeongoza ujumbe wa Tanzania katika
mkutano huo, amesema, hapana shaka kwamba ili
nchi iwe na takwimu sahihi, zenye viwango
vinavyokubaliwa kitaifa na kimataifa panahitajika ushirikiano baina ya
Idara za Kitaifa za Takwimu, Serikali na washirika wa
maendeleo.
“Upatikanaji wa takwimu zenye viwango katika utekelezaji wa
malengo ya maendeleo endelevu unatutaka tuwe wabunifu na tuboreshe
mifumo yetu ya takwimu. Na katika hili, tusijidanganye, haya yote
yanahitaji uwekezaji wa raslimali fedha na utaalam, patahitajika
ushirikiano ambao utasaidia kuimarisha takwimu na kusaidia utekelezaji wa
Agenda 2030”. Akaeleza Balozi Manongi.
Vilevile Mwakilishi huyo wa Tanzania, akaongeza kuwa
takwimu sahihi zina uwezo wa kuleta tofauti mkubwa kwa vile zinawasaidia
watendaji wa serikali katika upangaji wa sera na zinatoa ushahidi wa wapi
palipofanikiwa na wapi pana matatizo au mapungufu.Na akasisitiza
kwa kusema “ Takwimu sahihi zinasaidia uwazi na kubwa zaidi
uwajibikaji”.
Akizungumzia Zaidi nafasi ya takwimu sahihi na zenye viwango,
Balozi Manongi amesema, Tanzania inapenda kusisitiza tena umuhimu wa ukusanyaji
wa takwimu kuhusu idadi ya watu kwa kile anachosema ni nguzo
muhimu katika siyo tu ufuatiliaji wa utekelezaji wa maazimio ya
Mkutano wa Kimataifa wa Idadi ya watu na Maendeleo lakini pia utekelezaji
wa Ajenda 2030.
Akifafanua Zaidi kuhusu idadi ya watu, Balozi amesema, Tanzania ni kati
ya nchi zenye ongezeko kubwa la idadi ya watu na hususaji vijana
wanaoingia katika soko la ajira.“Ongezeko la vijana lina fursa na
changamoto pia. Tunatambua kwamba ili nchi yetu inufaike na uwepo wa
idadi kubwa ya vijana tunahitaji kuwa na mipango na sera madhubuti, ikiwa
ni pamoja na kuwapatia mafunzo na stadi ambazo zitaiwezesha serikali
kuvuna utaalamu na ujuzi wao” akabainisha Balozi.
Pamoja na ongezeko la idadi kubwa ya vijana, Balozi Manongi
amesema kuna ongezeko pia la wazee wa miaka 60 na kuendelea hali
inayoongeza mahitaji ya huduma za jamii na hususani afya. “ Ndiyo maana
tunatambua muingiliano wa idadi ya watu na maendeleo”.
Pamoja na kuzungumzia changamoto mbalimbali za ukusanyaji wa
takwimu sahihi na zenye ubora, Balozi amewaeleza wajumbe wa mkutano huo
kwamba, Serikali ya Tanzania imeendelea na juhudi za
kuiwezesha Idara ya Taifa ya Takwimu, ikiwa ni pamoja na
kuiwezesha kisheria kuwa chombo pekee chenye mamlaka ya
utoaji na usambazaji wa taarifa zinazohusiana na masuala ya takwimu.
Akatumia nafasi hiyo kutambua siyo tu mchango wa
serikali Kuu bali pia wadau mbalimbali wa maendeleo na ambao
wamekuwa wakisaidia katika eneo hilo.
Awali akifungua mkutano huo wa 49 wa Kamisheni ya Umoja wa
Mataifa ya Idadi ya Watu na Maendeleo.Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa Ban Ki Moon amesema watu wasipohesabiwa wanatengwa na
kwamba watu ni kiungo muhumu katika utekelezaji wa Agenda 2030.
Akaeleza malengo 17 ya maendeleo endelevu yamejikita
Zaidi katika usawa na kuwa takwimu za idadi ya watu, tathmini yake na
uchambuzi wake ni muhimu sana katika kumaliza au kupunguza tofauti ya kati ya
walionacho na wasionacho.Vilevile amesema takwimu sahihi zinasaidia katika
kuwasaidia na kuwafikia watu walioko katika maeneo ambayo yahafikiki na hivyo
kuwafikishia maendeleo na maisha yenye hadhi.

Comments
Post a Comment